Mapambano ya Wamasai wa Ngorongoro

Ambreena Manji anaandika kuhusu tishio la serikali ya Tanzania kuwaondoa Wamasai zaidi ya 80,000 kutoka Ngorongoro, mahali pa urithi wa dunia, nchini humo. Serikali inadai kwamba Wamasai lazima waondolewe kwenye ardhi yao kwa maslahi ya hifadhi na ekolojia ya makazi ya wanyamapori. Manji anaeleza nini hasa kinaendelea.

Na Ambreena Manji

Katika wiki za hivi karibuni, serikali ya Tanzania imerudia jitihada zake za kutenga ardhi katika kata ya Loliondo, wilayani Ngorongoro kaskazini wa nchi hiyo, kuwa ni makazi ya wanyamapori, na kimsingi kuwapiga marufuku Wamasai kwenye ardhi yao ya asili. Kama wafugaji wanaohamahama, maisha ya Wamasai hutegemea ufugaji wa ng’ombe na kilimo. Malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao ni muhimu kwao. Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa mahali pa urithi wa dunia palipotangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) tangu mwaka 1979. Lakini kwa muda mrefu, Wamasai wamekuwa wakikabiliwa na tishio la kuondolewa ili kupisha utalii na hifadhi ya wanyamapori.

Serikali imewatuhumu Wamasai kwa kuingilia njia za wanyamapori na maeneo ya wanyamapori kuzaliana na kudai kuwa kwa maslahi ya hifadhi ya wanyamapori na ekolojia, maeneo maalum kwa ajili ya wanyamapori lazima yaanzishwe kwenye ardhi hiyo ya Wamasai. Wamasai wamejipanga kupambana na hatua hizi, wakiishutumu serikali kwa kutumia hifadhi ya wanyamapori kama kisingizio cha kuwaondoa kwenye ardhi yao.

Hata hivyo, kulingana na Tanzania kuhurisha ardhi na kuvutia uwekezaji wa kigeni tangu miaka ya Tisini, imeelezwa kwamba sababu ya kurejea kwa hamu ya Ngorongoro ni mipango ya serikali kutoa vibali vya haki za uwindaji kwenye eneo lenye ukubwa wa maili za mraba 579 kwa wawekezaji wa kigeni. Kwa Wamasai, huu ni mwendelezo wa mwenendo wa muda mrefu tangu nchi ipate uhuru. Tangu wakati huo, Wamasai wamepoteza zaidi ya asilimia sabini ya ardhi yao kwa hifadhi. Mwaka 1992, mwekezaji kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) alipewa leseni ya uwindaji wa kitalii wa kuua wanyamapori katika eneo hilo. Mwaka 2018, ripoti moja ilieleza athari za makampuni binafsi katika maeneo hayo: kampuni ya Ortello Business Corporation iliwatimua Wamasai ili kuendesha kitalu cha uwindaji kwa ajili ya matumizi binafsi ya familia ya kifalme na wageni wao na iliendelea na shughuli zake katika eneo hilo baada ya leseni yao kuwa imefutwa na Wizara ya Maliasili ya Tanzania.

Chini ya himaya yenye jeuri ya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA), Wamasai wamekuwa na fursa ndogo ya ushiriki katika uendeshaji wa eneo hilo au maamuzi kuhusu mustakabali wao. NCAA inatuhumiwa kufanya shughuli zake kwa usiri. Inatoa taarifa kidogo tu kuhusu utekelezaji wa mpango mpya wa matumizi ya ardhi na makazi katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ambao utapelekea wakazi 80,000 kupoteza makazi, na kuvunjiwa nyumba zao, shule na miundombinu ya afya,

Kuakisi mapambano ya uainishaji na maana ya ardhi inayoonekana sehemu nyingine za Afrika Mashariki pindi jamii zinapoamua kulinda ardhi yao, wakazi wa Loliondo wanatoa hoja kwamba ardhi yenye mgogoro ni kijiji chini ya Sheria ya Vijiji ya mwaka 1999. Sheria hii ililenga kutoa mamlaka ya maamuzi kwa ngazi ya jamii. Wamasai wanadai kwamba ardhi yao ya asili itambulike kama kijiji halali na sio sehemu iliyotengwa kuwa hifadhi.

‘Hifadhi’

Katika kitabu chao muhimu cha mwaka 2017, The Big Conservation Lie (uongo mkubwa kuhusu hifadhi), John Mbaria na Mordecai Ogada wanabainisha ukweli dhidi ya maelezo yaliyotawala kuhusu hifadhi na kuchunguza unyonyaji mkubwa wa misitu ambayo wahifadhi wamekuwa wakidai wanailinda. Kurejea kwa uporaji ardhi unaovuka mipaka ya nchi unaoendelea Ngorongoro unathibitisha uchambuzi huu. Mwaka 2018, ripoti ya Taasisi ya Oakland ilionyesha jinsi sheria za hifadhi zilivyokuwa zinatumika kuwapora mali Wamasai. Kabla ya hapo, ripoti ya Wilbert Kapinga na Issa Shivji (ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Uchunguzi kwenye Masuala ya Ardhi) ilichunguza nguvu za kisheria na hatua za kiutawala za NCAA. Walionyesha vikwazo walivyowekewa Wamasai na NCAA bila majadiliano na ushiriki wa Wamasai katika mchakato wa maamuzi. Walipendekeza kwamba katika utawala wa NCAA kwenye Eneo la Hifadhi, uwakilishi stahili na ushiriki wa Wamasai na wakazi wengine ni muhimu ili waweze kuamua njia bora za hifadhi na kustawisha sehemu hiyo muhimu duniani.

Emutai

Jinsi wanavyotendewa Wamasai wa Ngorongoro inaonyesha aina flani na matendo yanatambulika kuwa ya kikoloni, kuwawekea mazingira ya maisha yanayoelekea kuondolewa kwa emutai. Katika Ki-Maa -lugha inayoongewa na Wamasai – neno emutai linamaanisha uharibifu au kuondoa na lilitumika kuelezea maradhi ya karne ya kumi na tisa ambapo nimonia inayoambukiza ya mifugo (bovine pleuropneumonia, sotoka (rinderpest) na ndui (smallpox) iliteketeza ng’ombe na kusababisha maradhi yaliyotapakaa. Ni neno lenye inayoakisi na haraka inayoongezeka. Mwaka 2018 Taasisi ya Oakland ilionya kwamba “bila kupata nafasi kwenye ardhi ya malisho na visima – bila uwezo wa kuzalisha chakula kwa ajili ya jamii, Wamasai wapo katika hatari ya kipindi kipya cha emutai.

Emutai ya sasa inajumuisha nini? Kwa sababu ya kutengwa upya kwa ardhi yao ambayo walikuwa wakiitumia kulisha ng’ombe na kupanda mazao, magonjwa na baa la njaa hutokea mara kwa mara. Wakilazimishwa kwenda kwenye maeneo madogo ya ardhi ili kutoa mwanya kwa utalii, uwezo wa Wamasai katika uzalishaji mali kijamii uliathiriwa sana: majukumu ya kila siku ya kulisha ng’ombe na kuzalisha chakula kwenye vitalu vidogo vya ardhi yamefanywa kutokuwa halali. Matokeo ni kusambaa kwa baa la njaa na magonjwa, hususan miongoni mwa watoto. Kuzingirwa kwa mabavu kwa ardhi yao kunawazuwia Wamasai kumudu maisha yao ya kila siku na kati ya vizazi. Kikwazo hiki kwa uzalishaji mali kijamii kwa Wamasai ni tishio halisi. Ardhi iliyomegwa kama sehemu ya uzalishaji mali na urithi wa asili, Wamasai wanakumbana na mateso yanayotokana na jitihada za serikali kuwaridhisha matajiri na watu maarufu wanaokuja Kutalii Ngorongoro. Katika maneno ya kiongozi wa Wamasai, Julius Peter Olekitika, “fikiria nyumba yako inachomwa moto mbele yako ili kutoa nafasi kwa wageni kutoka nje kuwinda wanyamapori. Fikiria kutoweza kulisha ng’ombe wetu kwa sababu serikali inataka kumlinda mwekezaji kutoka nje ambaye maslahi yake pekee ni kuwinda wanyamapori.”

Athari pana

Mapambano ya Wamasai wa Ngorongoro ina umuhimu mkubwa katika kuelewa jinsi gani “utengaji maeneo ya hifadhi kwa kuwaondoa kwa nguvu au kutowashirikisha wakazi wa eneo husika” unavyofanya kazi na unavyoondoa nafasi ya wazawa kama wasimamizi wa ardhi husika. Hii ni muhimu katika nyakati za changamoto ya hali ya hewa. Aina za ukoloni mamboleo kwenye hifadhi huambatana na uhusiano kati ya vyombo vya dola na uhifadhi (vitisho na matumizi ya wanamgambo ni mambo yaliyozoeleka) na kwa uhusiano na makampuni ya kimataifa ya fueli za kisukuku.

Nchini Tanzania, serikali na makampuni binafsi wanakula njama. Kinyume na madai ya uhifadhi, lengo ni kubomoa kwa makusudi maisha ya Wamasai, kubaki tu na vitu vitakavyoendana na malengo ya utalii kupitia kuwafanya watu kama vivutio vya utalii, mantiki ya kibaguzi ya ukoloni wa walowezi. Kama Taasisi ya Oakland inavyotambua, hii haitoishia wao kuondolewa kwenye ardhi lakini pia kuwaondoa uhai.

Wilbert Kapinga na Issa Shivji wanajadili kwenye ripoti yao kwamba mapambano ya Wamasai wa Ngorongoro yasichukuliwe kama mapambano ya wachache bali yachochee kuanzishwa kwa ushirikiano kati ya wananchi wote wanaokabiliwa na tishio la kuporwa ardhi na kutokuwa na ardhi kutokana na sheria mpya ya ardhi (Sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999).

Kuchambua athari za kisiasa za kuwaangalia Wamasai kama kundi dogo au wazawa kama yanavyofanya makundi mengi ya utetezi ya kimataifa, walipinga matumizi ya neno hilo, wakidai kwamba itakuwa na athari muhimu kwa asasi za kiraia. Waandishi wamejenga hoja kwamba hilo halijapewa mkazo. Kwa kuwatenganisha Wamasai na wananchi wengine, watakuwa wametengwa na jamii nzima.

Hoja hii muhimu inatuhamasisha kutafiti uzoefu wa pamoja wa kuondolewa kwa nguvu kwa muktadha wa maeneo ya mijini na vijijini, kutambua uhalisi wao na historia zao, huku ukitafutwa ushirikiano mbali zaidi ya muktadha wa kila kuondolewa kwa nguvu au tishio la kukosa makazi. Hakuna shaka kuwa Wamasai wanatengwa na kufanyiwa ubaguzi wa kutisha na serikali, vitendo vinavyoungwa mkono na kampeni mahsusi za chuki. Jukumu ni kueleza mapambano yao na yale ya wengine wanaoishi na tishio la kuporwa mali zao. Kama Salar Mohandesi na Emma Teitalman wanavyotukumbusha katika insha yao ya Without Reserves (bila hifadhi), ni lazima tutambue “aina mbalimbali ya maeneo yaliyotengwa”: wakazi wa mijini hawaepuki miondoko ya maeneo yaliyotengwa ambayo huathiri maisha yao.

Kumekuwa na wito kadhaa wa kuundwa tume ya uchunguzi kuhusu Ngorongoro. Katika hilo, ninashauri ufafanuzi wa hoja ya Wilbert Kapinga na Issa Shivji hapo juu: sasa ni wakati mwafaka kwa harakati za kijamii na vikundi vya asasi za kiraia zinazojihusisha na kupinga kuondolewa kwa nguvu – iwe mijini au vijijini – kuwaunga mkono Wamasai. Ni lazima tuunganishe Wamasai kuporwa mali na athari pana za uhurishaji wa sheria za ardhi na kukua kwa uporaji wa ardhi nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Ambreena Manji ni Profesa wa Sheria za Ardhi na Maendeleo katika Chuo Kikuu cha Cardiff, Shule ya Sheria na Siasa. Ni mwandishi wa kitabu The Struggle for land and justice in Kenya (mapambano ya ardhi na haki Kenya) (James Currey/Brewer & Boydell 2020; Vita Books 2021)

Pichani: Zaidi ya Wamasai 700 walikusanyika katika kijiji cha Oloirobi mnamo Februari 13, 2022 ili kuomba dhidi ya kufurushwa kutoka kwa ardhi ya mababu zao. (Taasisi ya Oakland).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.